WAHAMIAJI
haramu 194 waliorudishwa makwao wakati wa kutekeleza awamu ya kwanza ya
Operesheni Kimbunga iliyoisha mwishoni mwa wiki iliyopita, wamekataliwa
na nchi zao na kurejeshwa tena nchini. Mamlaka zinazohusika na
operesheni hiyo zimesema kuwa wamewapokea tena watu hao wakati
wanasubiri hatua za kisheria kuchukuliwa.
Awamu
ya kwanza ya operesheni hiyo ilianza Septemba 6 na kuhitimishwa
Septemba 20 mwaka huu baada ya baadhi ya wahamiaji haramu, kukaidi mwito
wa Rais Jakaya Kikwete wa kurejea makwao na kama wanataka kurudi,
wafuate utaratibu wa Sheria.
Taarifa
iliyotolewa na Naibu Kamishna wa Polisi, Simon Sirro, ilieleza kuwa
watu hao pamoja na kutokuwa na sifa ya kuwa raia wa Tanzania,
wamerejeshwa nchini kwa kuwa pia wamekosa sifa ya kuwa raia wa nchi
jirani ambako Serikali iliwapeleka baada ya vigezo kuthibitisha kuwa ni
raia wa nchi hizo.
"Hadi
kufikia mwisho wa Awamu ya Kwanza wa Operesheni hii, timu ya Operesheni
imefanikiwa kukamata wahalifu wa unyang’anyi wa kutumia silaha pamoja
na washirika wao na kuhakiki uraia wa watuhumiwa wa uhamiaji haramu,"
alisema Sirro.
Kwa
mujibu wa Sirro, kati ya waliokamatwa wapo watuhumiwa 212 wa
unyang’anyi wa kutumia silaha na majangili ambao ni raia wa Tanzania 23.
Silaha
Silaha zilizokamatwa ni mabomu 10 ya kutupwa kwa mkono, silaha 61
zikiwemo bunduki aina ya SMG (50, Shotgun (8), Mark IV (1), Riffle (1),
pistol (1), pisto za kienyeji (3) na magobori 42 pamoja na mitambo
miwili ya kutengeneza silaha aina ya magobori.
Zingine
ni risasi 665 zikiwemo za bunduki aina ya SMG na SAR risasi 561,
shotgun risasi 22, gobori risasi 82 na fataki 8, suruali sare za Jeshi
na kibuyu cha maji vya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania. Sirro
aliongeza kuwa wahamiaji haramu 12,704 wamekamatwa, kati yao Wanyarwanda
3,448, Warundi 6,125, Waganda 2,496, Wakongo 589 Wasomali 44, Myemeni
mmoja na raia wa India mmoja.
“Wahamiaji
haramu 2,129 walikubali kuondoka nchini kwa hiari yao; 8,696
waliondoshwa nchini kwa amri ya Mahakama baada ya kupewa hati ya
kufukuzwa nchini na 1,852 waliachiwa huru baada ya Serikali kuthibitisha
uraia wao wakati wengine 2,286 wanaendelea na mahojiano ili
kuthibitisha uraia wao,” alisema.
Kiongozi
huyo wa operesheni alisema ng’ombe 8,226 walikamatwa wakiwa wanachungwa
katika hifadhi za misitu na Sh milioni 32.5 zimepatikana, ikiwa ni tozo
za faini ya ng’ombe walioachwa kwenye hifadhi ya Taifa.
Vingine
vilivyokamatwa ni ngozi za wanyama aina ya duma (1), swala (2), nyati
(1) na vipande 10 vya nyama vinavyodhaniwa kuwa nyara za Serikali.
Vingine
vilivyokamatwa ni vipande viwili vya meno ya tembo pamoja na mbao
2,105, magogo 86, mkaa magunia 467, pombe haramu ya gongo lita 375 na
mtambo wa gongo mmoja . Pia wamekamata bangi kilo 77 na makokoro
yanayotumika kuvua samaki kinyume cha sheria.
"Takwimu
zinaonesha kuwa Mkoa wa Kagera unaongoza kwa kukamata wahamiaji haramu
7,001, ukifuatiwa na mkoa wa Kigoma uliokamata wahamiaji haramu 5,005
wakati mkoa wa Geita wahamiaji haramu waliokamatwa walikuwa 698," alisema Sirro.
Sirro
alisema pamoja na mafanikio yaliyopatikana, kumekuwepo na changamoto
zilizojitokeza, ikiwa ni pamoja na hali ya maisha mchanganyiko ya
Watanzania asilimia 60 na wahamiaji asilimia 40 katika mikoa ya mpakani.
Alitaja
changamoto nyingine kuwa ni baadhi ya wananchi wenye nia mbaya au
kulipizana visasi, waliotaka kutumia operesheni hiyo kukomoana kwa
kuwataja baadhi ya watu kuwa ni wahalifu kumbe ni uongo.
Nyingine
ni baadhi ya wahamiaji baada ya kukamatwa walikosa sifa za uraia wa
Tanzania na hata waliporudishwa kwenye nchi wanazodhaniwa kutoka,
walikosa sifa za uraia na kuleta mgongano kuhusu uraia wao. Alisema
ukosefu wa vitambulisho vya uraia ulisababisha ugumu wa kutambua
wahamiaji haramu.
Pia
kutokuwepo kwa uzio katika mipaka ya nchi yetu, kumesababisha wahamiaji
haramu wanapopelekwa kwao, kurudi kupitia njia za panya. Matarajio
Sirro alisema baada ya kukamilisha Awamu ya Kwanza ya Operesheni
Kimbunga, wanatarajia Serikali itashughulikia changamoto zilizojitokeza,
ili kupunguza baadhi ya matatizo katika mikoa ya Kagera, Kigoma na
Geita hususan yanayohusu uhalifu na masuala ya kiuhamiaji.
"Tunatarajia
kuanzisha kikosi kazi kila mkoa, kwa ajili ya ufuatiliaji wa wahalifu
sugu wanaotumia silaha za kivita na wale wanaowafadhili," alisema Sirro.
Alisema
uhamasishaji utafanyika kuanzia ngazi ya familia, kitongoji,
mtaa/kijiji, kata, tarafa, wilaya mkoa na taifa, ili jamii iimarishe
misingi ya ulinzi na usalama kupitia kamati zilizopo na kutoa taarifa
mara moja panapojitokeza jambo lolote linalohusu ulinzi na usalama
katika maeneo yao.
Alisisitiza
kuwa watajipanga kimkakati, ili kuona namna ya kushughulikia baadhi ya
wahamiaji haramu waliokosa sifa za uraia na kurudishwa nchini mwao,
ambao wanang’ang’ania kwa kusema wao ni Watanzania.
-----HABARI LEO