Monday, September 23, 2013

WAHAMIAJI HARAMU WAKATALIWA MAKWAO



WAHAMIAJI haramu 194 waliorudishwa makwao wakati wa kutekeleza awamu ya kwanza ya Operesheni Kimbunga iliyoisha mwishoni mwa wiki iliyopita, wamekataliwa na nchi zao na kurejeshwa tena nchini. Mamlaka zinazohusika na operesheni hiyo zimesema kuwa wamewapokea tena watu hao wakati wanasubiri hatua za kisheria kuchukuliwa.
Awamu ya kwanza ya operesheni hiyo ilianza Septemba 6 na kuhitimishwa Septemba 20 mwaka huu baada ya baadhi ya wahamiaji haramu, kukaidi mwito wa Rais Jakaya Kikwete wa kurejea makwao na kama wanataka kurudi, wafuate utaratibu wa Sheria.
Taarifa iliyotolewa na Naibu Kamishna wa Polisi, Simon Sirro, ilieleza kuwa watu hao pamoja na kutokuwa na sifa ya kuwa raia wa Tanzania, wamerejeshwa nchini kwa kuwa pia wamekosa sifa ya kuwa raia wa nchi jirani ambako Serikali iliwapeleka baada ya vigezo kuthibitisha kuwa ni raia wa nchi hizo.
"Hadi kufikia mwisho wa Awamu ya Kwanza wa Operesheni hii, timu ya Operesheni imefanikiwa kukamata wahalifu wa unyang’anyi wa kutumia silaha pamoja na washirika wao na kuhakiki uraia wa watuhumiwa wa uhamiaji haramu," alisema Sirro.
Kwa mujibu wa Sirro, kati ya waliokamatwa wapo watuhumiwa 212 wa unyang’anyi wa kutumia silaha na majangili ambao ni raia wa Tanzania 23.
Silaha Silaha zilizokamatwa ni mabomu 10 ya kutupwa kwa mkono, silaha 61 zikiwemo bunduki aina ya SMG (50, Shotgun (8), Mark IV (1), Riffle (1), pistol (1), pisto za kienyeji (3) na magobori 42 pamoja na mitambo miwili ya kutengeneza silaha aina ya magobori.
Zingine ni risasi 665 zikiwemo za bunduki aina ya SMG na SAR risasi 561, shotgun risasi 22, gobori risasi 82 na fataki 8, suruali sare za Jeshi na kibuyu cha maji vya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania. Sirro aliongeza kuwa wahamiaji haramu 12,704 wamekamatwa, kati yao Wanyarwanda 3,448, Warundi 6,125, Waganda 2,496, Wakongo 589 Wasomali 44, Myemeni mmoja na raia wa India mmoja.
“Wahamiaji haramu 2,129 walikubali kuondoka nchini kwa hiari yao; 8,696 waliondoshwa nchini kwa amri ya Mahakama baada ya kupewa hati ya kufukuzwa nchini na 1,852 waliachiwa huru baada ya Serikali kuthibitisha uraia wao wakati wengine 2,286 wanaendelea na mahojiano ili kuthibitisha uraia wao,” alisema.
Kiongozi huyo wa operesheni alisema ng’ombe 8,226 walikamatwa wakiwa wanachungwa katika hifadhi za misitu na Sh milioni 32.5 zimepatikana, ikiwa ni tozo za faini ya ng’ombe walioachwa kwenye hifadhi ya Taifa.
Vingine vilivyokamatwa ni ngozi za wanyama aina ya duma (1), swala (2), nyati (1) na vipande 10 vya nyama vinavyodhaniwa kuwa nyara za Serikali.
Vingine vilivyokamatwa ni vipande viwili vya meno ya tembo pamoja na mbao 2,105, magogo 86, mkaa magunia 467, pombe haramu ya gongo lita 375 na mtambo wa gongo mmoja . Pia wamekamata bangi kilo 77 na makokoro yanayotumika kuvua samaki kinyume cha sheria.
"Takwimu zinaonesha kuwa Mkoa wa Kagera unaongoza kwa kukamata wahamiaji haramu 7,001, ukifuatiwa na mkoa wa Kigoma uliokamata wahamiaji haramu 5,005 wakati mkoa wa Geita wahamiaji haramu waliokamatwa walikuwa 698," alisema Sirro.
Sirro alisema pamoja na mafanikio yaliyopatikana, kumekuwepo na changamoto zilizojitokeza, ikiwa ni pamoja na hali ya maisha mchanganyiko ya Watanzania asilimia 60 na wahamiaji asilimia 40 katika mikoa ya mpakani.
Alitaja changamoto nyingine kuwa ni baadhi ya wananchi wenye nia mbaya au kulipizana visasi, waliotaka kutumia operesheni hiyo kukomoana kwa kuwataja baadhi ya watu kuwa ni wahalifu kumbe ni uongo.
Nyingine ni baadhi ya wahamiaji baada ya kukamatwa walikosa sifa za uraia wa Tanzania na hata waliporudishwa kwenye nchi wanazodhaniwa kutoka, walikosa sifa za uraia na kuleta mgongano kuhusu uraia wao. Alisema ukosefu wa vitambulisho vya uraia ulisababisha ugumu wa kutambua wahamiaji haramu.
Pia kutokuwepo kwa uzio katika mipaka ya nchi yetu, kumesababisha wahamiaji haramu wanapopelekwa kwao, kurudi kupitia njia za panya. Matarajio Sirro alisema baada ya kukamilisha Awamu ya Kwanza ya Operesheni Kimbunga, wanatarajia Serikali itashughulikia changamoto zilizojitokeza, ili kupunguza baadhi ya matatizo katika mikoa ya Kagera, Kigoma na Geita hususan yanayohusu uhalifu na masuala ya kiuhamiaji.
"Tunatarajia kuanzisha kikosi kazi kila mkoa, kwa ajili ya ufuatiliaji wa wahalifu sugu wanaotumia silaha za kivita na wale wanaowafadhili," alisema Sirro.
Alisema uhamasishaji utafanyika kuanzia ngazi ya familia, kitongoji, mtaa/kijiji, kata, tarafa, wilaya mkoa na taifa, ili jamii iimarishe misingi ya ulinzi na usalama kupitia kamati zilizopo na kutoa taarifa mara moja panapojitokeza jambo lolote linalohusu ulinzi na usalama katika maeneo yao.
Alisisitiza kuwa watajipanga kimkakati, ili kuona namna ya kushughulikia baadhi ya wahamiaji haramu waliokosa sifa za uraia na kurudishwa nchini mwao, ambao wanang’ang’ania kwa kusema wao ni Watanzania.
-----HABARI LEO

No comments:

Post a Comment