KESI ya kutorosha wanafunzi inayomkabili
Mchungaji wa Kanisa la Tanzania Assemblies Of God (TAG), Jean Felix
Bamana, Raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Jumatatu wiki
hii ilianza kurindima katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi,
Kilimanjaro huku upande wa walalamikaji ukiiambia korti, ‘mchungaji
alitaka penzi bila kinga’.
Mchungaji huyo alitiwa mbaroni Machi 13,
mwaka huu ndani ya Hoteli ya Grand iliyopo Magomeni, Dar akiwa na
wanafunzi wawili, watoto wa familia moja, Artha Swai (17) na Angel Swai
(19) ambao alidaiwa kuwatorosha kutoka mjini hapa.
Katika kesi ya
msingi, mchungaji huyo alidaiwa kuwadanganya watoto hao kwamba alikuwa
akiwafanyia mpango wa kwenda kusoma nje ya nchi lakini badala yake
aliwaweka hotelini na kumtaka kimapenzi mmoja wao
SAA 3:30 ASUBUHI AFIKISHWA MAHAKAMANI
Akiwa
chini ya ulinzi mkali wa polisi, Amani lilimshuhudia Mchungaji Bamana
ambaye alishindikana kufikishwa mahakamani mara tatu mfululizo kwa
visingizio vingi, akipandishwa kizimbani huku akikwepa macho ya umati
uliofurika kufuatilia kesi hiyo.
MASHITAKA
Akisoma
mashitaka yanayomkabili Mchungaji Bamana katika Mahakama ya Hakimu
Mkazi Moshi, mbele ya Hakimu Naomi Mwerinde, mwendesha mashitaka ambaye
ni wakili wa serikali, Abdallah Chavula alisema mtuhumiwa huyo
anashitakiwa kwa makosa mawili.
Chavula alisema, katika makosa hayo,
la msingi ni la kutorosha wanafunzi kinyume na Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania chini ya sheria namba 6 ya mwaka 2008, ibara ya 4, kifungu cha
5, kifungu kidogo 4 (i)a.
Katika mashitaka hayo, ilidaiwa
mahakamani hapo kuwa, mnamo Februari 18, mwaka huu, Angel ambaye
kipindi hicho alikuwa ni mwanafunzi wa kidato cha tano katika Shule ya
Sekondari ya Mtakatifu Marygorethi ya mkoani hapa, akiwa nyumbani kwao
eneo la Masama wilayani Hai, alimuomba mdogo wake, Artha amsindikize
mjini Moshi.
Mwendesha mashitaka huyo aliendelea kufafanua mbele ya
mahakama hiyo kuwa, wanafunzi hao waliondoka nyumbani bila kutoa
taarifa na kwamba walifikia Moshi View Hotel ambako walikutana na
mshitakiwa huyo.
Ilidaiwa kortini hapo kuwa wakati watatu hao
wakifanya mazungumzo, Artha alimueleza mshitakiwa dhamira yake ya
kuendelea na masomo baada ya kumaliza kidato cha nne na mtuhumiwa
alimhakikishia kwamba kwa kuwa ni mtu wa kuzuguka kila mahali duniani
kote angemsaidia kupata shule nje ya nchi.
Ilielezwa kuwa kama
ilivyokuwa kwa mdogo wake, Angel naye alihakikishiwa kufanyiwa
utaratibu wa kupata shule nje ya nchi ambapo mshitakiwa alimuahidi
kumpeleka Uingereza kusomea masuala ya ubunifu na mitindo.
Mwendesha
mashitaka huyo aliiambia mahakama kuwa majira ya saa tisa alasiri,
mshitakiwa aliwapa nauli ya teksi kutoka Moshi kuwarudisha nyumbani
Masama na kwa kuwa waliondoka bila kuaga, bibi yao aliwagombeza.
Chavula
aliendelea kuiambia mahakama kuwa, katika mawasiliano kati ya watatu
hao, Mchungaji Bamana alikuwa akimsisitiza Angel afanye uamuzi mgumu wa
kuondoka nyumbani kwao na kumfuata Dar kwa sababu wazazi wake (Angel),
watakufa muda wowote, yeye na mdogo wake watapata matatizo kama
watakuwa hawawezi kujitegemea.
ZAWADI YA SIMU
Mahakama
iliendelea kuelezwa kuwa siku ya kwanza kukutana, mshitakiwa alimpa
Artha simu ya Samsung Touch Screen na kwamba siku iliyofuata, mtuhumiwa
alimpigia simu Angel kupitia simu aliyompa Artha na kuwataka waende
mjini wakale naye bata.
Angel na mdogo wake walitoroka nyumbani kwa
kutumia usafiri wa teksi ya mtu aliyefahamika kwa jina moja la Yusuf
ambapo baada ya kufika mjini walikutana na mchungaji huyo aambaye
aliwapeleka Nakumatt Supermarket alipowanunulia biskuti na headphone za
simu.
SMS ZA MAPENZI
Mahakama
ilielezwa kuwa, pande zote ziliendelea kupigiana simu na kutumiana
ujumbe mfupi (SMS) na katika mazungumzo, mshitakiwa aliendelea
kuwasisitiza Angel na Artha kutoroka nyumbani na kuongeza kuwa siku
iliyofuata mshitakiwa aliondoka kurejea Dar.
ARTHA AMFUATA MCHUNGAJI DAR
Hakimu
Mwerinde aliambiwa kuwa, Februari 18, mwaka huu, Artha alimuaga baba
yake kuwa anakwenda Machame kumsalimia bibi yake lakini badala yake
alikwenda Moshi kukata tiketi ya basi la saa sita linalokwenda Dar.
Majira
ya Saa 7:00 mchana, Artha alimpigia simu Angel kumfahamisha juu ya
safari yake na baadaye akawasiliana na mshitakiwa na kwamba mtuhumiwa
alimuagiza akifika Ubungo achukue teksi hadi Grand Hotel ya Magomeni.
Baada
ya kufika hotelini hapo, Artha alipokelewa na mshitakiwa na kwa pamoja
waliingia mapokezi ambapo mtuhumiwa huyo alilipia gharama zote za
malazi ya kijana huyo huku akimhakikishia kufuatilia taratibu za kupata
hati ya kusafiria siku inayofuata.
ANGEL NAYE ATIMKIA DAR
Mwendesha
Mashitaka Chavula aliendelea kuieleza mahakama kuwa, siku mbili baada
ya Artha kufika Dar, Februari 20, Angel alitumiwa shilingi laki moja
kwa mtandao kupitia simu ya dereva teksi.
Katika fedha hizo, Sh.
40,000 alitumia kama nauli ya teksi kumtoa Masama hadi Moshi Mjini na
zilizosalia, Sh. 60,000 zilitumika kwa nauli ya kwenda Dar.
Chavula
alidai kuwa Angel alitumia Sh. 18,000 kukata tiketi ya basi na kwamba
mara tu baada ya kufika Dar, alipokelewa na mshitakiwa huyo katika
Hoteli ya Grand.
MCHUNGAJI ATAKA PENZI BILA KINGA
Katika
jambo lililoshtua wengi mahakamani hapo ni pale mwendesha mashitaka
huyo alipoiambia korti kuwa mshitakiwa alitaka penzi kwa Angel.
Alisema
kuwa katika harakati za kufanikisha azma yake ya kufanya mapenzi na
Angel, mchungaji Bamana alikuwa akishinda kutwa katika chumba cha
msichana huyo.
Ilidaiwa kuwa mchungaji huyo alikuwa akimshawishi Angel kwa njia zote kufanya naye mapenzi bila kinga!
Mwendesha
mashitaka huyo alisema kuwa mara zote, Angel alikataa na kumshauri
mchungaji kuwa kama anataka kufanya naye mchezo huo mchafu basi atumie
kinga, kitu ambacho mchungaji huyo hakuwa tayari kukifanya.
Ilielezwa
kuwa baada ya kugonga mwamba kupata penzi, mchungaji aliambulia
kumshikashika na kumbusu mara kwa mara, kitendo kilichomfanya mdogo wake
Angel, Artha aanze kuingiwa na shaka pamoja na kwamba walikuwa
wakitarajia kusaidiwa.
MCHUNGAJI AKANA MASHITAKA
Upande
wa mshitakiwa ulipotakiwa kuwasilisha utetezi wa mashitaka yote
mawili, mshitakiwa akiongozwa na mawakili wawili, Erick Gabriel na
Rongino Myovela pamoja na kukubaliana na maelezo lakini walikana
mashitaka yote.
MASHAHIDI
Kutokana
na ugumu wa shitaka hilo, mwendesha mashitaka baada ya kushauriana na
mawakili wa mchungaji, aliiomba mahakama iahirishe zoezi la kusikilizwa
kwa kesi hadi pale upande wa mshitakiwa utakapopeleka mashahidi nane
na vielelezo.
Baada ya kujiridhisha na maelezo ya upande wa
mashitaka na kukubaliana na ombi la mwendesha mashitaka, Hakimu
Mwerinde aliahirisha kesi hiyo hadi Juni 3, mwaka huu itakaposikilizwa
tena.
No comments:
Post a Comment