Tuesday, July 23, 2013

MAFUTA YA UBUYU YAZUA MAPYA TENA....ALBINO WAKATAZWA KUYATUMIA KWAAJILI YA NGOZI ZAO..!!

BAADHI ya wagonjwa wa Saratani waliolazwa katika Taasisi ya Saratani Ocean Road mjini Dar es Salaam, wamebainika wanatumia mafuta ya ubuyu wakati yanadaiwa kusababisha saratani ya ini. Uchunguzi uliofanywa na MTANZANIA katika taasisi hiyo, umebaini wagonjwa wengi wanatumia mafuta hayo kwa usiri mkubwa. Katika hatua nyingine, Chama cha Albino Tanzania (TAS), kimewataka watu wenye ulemavu wa ngozi (albino), wanaotumia mafuta hayo kuacha mara moja, hadi hapo Serikali itakapotoa taarifa rasmi kuhusu matumizi ya mafuta hayo kwa ngozi ya albino.

Katika uchunguzi huo, imebainika baadhi ya albino hutumia mafuta hayo kwa kujipaka huku wengine wakiwa na vidonda kwenye ngozi zao.

Akizungumza na MTANZANIA, Katibu wa Chama hicho Taifa, Ziyada Nsembo alisema, TAS hakina elimu kuhusu bidhaa hiyo, hivyo wanaotumia wanaweza kuathiri ngozi zao zaidi.

Tunawataka albino wanaotumia mafuta haya waache mpaka Serikali itakapotoa tamko rasmi kuwa mafuta hayo hayana athari kwa ngozi ya albino.

“Ngozi ya albino ni nyepesi, ina uwezo mkubwa wa kupitisha kemikali ndani ya mwili, ikiwa hayafai kunywa basi kwetu hayafai hata kujipaka, maana wengine wana vidonda. 


“Tumeamua kutoa kauli hii kwa sababu kuna mafuta ambayo albino hatakiwi kupaka mchana, huwa hayana uwezo wa kukinga mionzi ya jua. 

Haya mafuta ya ubuyu tunaelezwa kuwa yanalainisha ngozi, hatujui kama yanakinga ya mionzi ya jua, hilo ndilo tatizo letu, tunashauri yasitumike hadi wataalamu wa masuala ya ngozi ya albino watufahamishe,” alisema Katibu huyo.

Mmoja wa albino ambaye ni kiongozi, alisema ameshawahi kutumia mafuta hayo.

Wapo albino wanaotumia haya mafuta, hata mimi ni mmoja wapo, ila sikujua kama yana madhara, kwa sasa nimeacha kutumia.”

No comments:

Post a Comment