Tuesday, July 23, 2013 | 12:45 PM
Jeshi la Polisi Kanda Maalumu Dar es
Salaam, limepeleka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali maji yanayodhaniwa kuwa
ni tindikali aliyomwagiwa mmiliki wa maduka ya Home Shopping Center
(HSC), Said Mohammed Saad kwa ajili ya uchunguzi.
Mmoja wa Ofisa wa Polisi, ambaye
hakutaka kutaja jina lake aliliambia gazeti hili jana kuwa baada ya
tukio hilo polisi wameamua kuyachukua maji hayo na kuyapeleka huko kwa
uchunguzi ili kubaini ndani yake yalikuwa na nini.
Tukio hilo la kumwagiwa maji hayo
lilitokea Julai 20 mwaka huu saa 1 usiku karibu na Kituo cha Polisi cha
Osterbay wilayani Kinondoni, wakati Saad akizungumza na mmoja wa
wafanyakazi wake katika duka lake jipya lililopo katika maeneo hayo.
“Majibu yatakayotoka kwa Mkemia Mkuu yatatusaidia katika upelelezi wetu katika jambo hili,” alisema Ofisa huyo na kuongeza kuwa.
“Hadi sasa hakuna mtu yeyote anayeshikiliwa kutokana na tukio hili huku polisi wakiendelea na msako mkali wa kuwabaini wahusika.”
Alidokeza kuwa kwa mujibu wa ndugu wa
karibu wa Saad wanasema mgonjwa wao anaendelea vizuri na matibabu
katika moja ya hospitali aliyolazwa, huku polisi wakimsubiri apate
ahueni kwa ajili ya kumfanyia mahojiano juu ya tukio hilo.
Katika hatua nyingine, polisi kanda
hiyo leo wanatarajia kufanya mkutano na waandishi wa habari kutoa
ufafanuzi kuhusu suala kulipuka kwa bomu katika mkutano wa Chadema.
Tukio hilo lilitokea Julai 22 mwaka huu
maeneo ya Viwanja vya Sahara Mabibo wakati kitu kinachodhaniwa ni bomu
kilichokuwa ndani ya gari la polisi kilirushwa katika mkutano huo.
No comments:
Post a Comment