Tuesday, July 23, 2013

WAJANE WA WANAJESHI WA JWTZ WALIOUAWA HUKO DARFUL WAILILIA SERIKALI....!!

WAJANE wa askari saba wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), wameililia Serikali iwasaidie kuwajengea nyumba za kuishi, ili kuepuka matatizo ya kifamilia ambayo yanaweza kuwapata baada ya kufiwa. Mbali ya kuomba msaada huo, wajane hao pia wameiomba Serikali iwasaidie kusomesha watoto wao kutokana na uwezo kuwa mdogo. 


Wakizungumza kwa uchungu kwa nyakati tofauti jana, wakati wa kuaga miili saba ya askari hao, katika viwanja vya makao makuu ya JWTZ Upanga, Dar es Salaam, wajane hao wamesema wamebaki katika wakati mgumu wa kukabiliana na maisha.

Mmoja wa wajane hao, Mariam Masudi (30), ambaye aliolewa na marehemu Sajenti Shaibu Salehe Othman na kufanikiwa kuzaa naye watoto wanne, ambao ni Salma Shaibu ambaye anasoma kidato cha nne, Nadhira Shaibu (darasa la sita), Ilham Shaibu (darasa la pili) na Abdulhakim Shaibu (chekechea), akielezea masikitiko yake yakuondokewa na mume wake alisema:

Nina uchungu sana wa kuondokewa na mwenzangu, nilikuwa namtegemea mume wangu kwa kila kitu.

“Naomba jeshi, linisaidie kusomesha watoto wangu…tumesikia tutapewa fedha, lakini nakwambia nyumba ndiyo itakuwa sehemu ya kutuenzi na watoto wangu,” alisema huku akibubujikwa na machozi.


Naye, mjane Maria Reston (30), ambaye alikuwa ameolewa na Koplo Oswald Chaula alisema anaishi katika nyumba za jeshi katika kota za Chabuluma mkoani Ruvuma, ameachwa na watoto wanne.

Msiba huu, unaniuma sielewi mume wangu amekufaje jamani, kwa kuwa imetokea namwachia Mungu.

“Taarifa za vifo vya wanajeshi nilizipata kwenye magazeti, sijui kwanini nilihisi mume wangu atakuwa miongoni mwao.

“Niliposoma nikaona jina la mume wangu, siamini kama kweli mume wangu amefariki jamani,” alisema Maria kwa uchungu.


Aliwataja watoto wake, kuwa ni Elizabeth Chaula (anasoma kidato cha kwanza), Clares (darasa la sita), Eliud (darasa la kwanza) na Joshua (ana umri wa miezi 10).

No comments:

Post a Comment