Mtoto Fahad Jamal (7) ambaye hali
yake ilikuwa mbaya na kulazwa chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi
maalumu (ICU) katika Hospitali ya Selian kufuatia kujeruhiwa na bomu
katika mkutano wa Chadema Arusha, amefariki dunia juzi saa saba mchana
hospitalini hapo.
Kwa mujibu wa Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo, Dk Paul Kisanga mtoto huyo alifariki dunia
wakati timu ya madaktari kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MOI) na Hospitali ya Jeshi ya Lugalo, Dar es Salaam wakijitahidi kila hali kuokoa maisha yake.
Kifo hicho kinaongeza idadi ya marehemu na kuwa wanne baada ya vifo vya Amiri Ally (7), Judith Moshi (25) ambaye ni Katibu wa Baraza la Wanawake Chadema (BAWACHA)Kata ya Sokoni One jijini Arusha na Ramadhan Juma (15).
Dk Kisanga alisema hospitali hiyo juzi ilipokea majeruhi wengine 17 wa mabomu ya kutoa machozi katika eneo la Soweto wakati polisi wakitawanya wafuasi wa Chadema.
Alisema majeruhi 14 wamelazwa huku watatu wakitibiwa na kuruhusiwa ambapo pia Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari aliyekuwa amelazwa hapo kutokana na kuumia shingoni aliruhusiwa na hali yake inaendelea vizuri.
Wakati hayo yakijiri, Kamanda wa Operesheni Maalumu wa Jeshi la Polisi, Paul Chagonja amemtaka Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na Mwanasheria wa Chama hicho, Tundu Lissu ambaye pia ni mbunge kupeleka ushahidi wao kwa Mkuu wa Nchi.
Chagonja alisema hayo jana mjini hapa akizungumza na waandishi wa habari akisisitiza kuwa kama Mbowe , Lissu na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema hawana imani na Polisi na kuituhumu kuwa mtuhumiwa namba moja wa mlipuko wa bomu Jumamosi jijini hapa, basi ushahidi wao wampelekee Rais.
Alisema lakini litakuwa jambo la kushangaza wabunge hao kukataa kutoa ushahidi Polisi wachunguze tukio hilo lililosababisha vifo vya watu watatu na kupelekea baadhi ya watu kujeruhiwa.
Aliongeza kuwa kuna baadhi ya watu hawapendi kuona Arusha na nchi inakuwa na amani akawasihi Watanzania kutokubali amani iliyopo kuvurugwa na watu wachache.
"Natoa mwito kwa viongozi hao watuletee ushahidi huo huku Lema na Mbowe wakijisalimisha Polisi bado tunashikilia watu watatu ambao hatujawapeleka mahakamani wanaendelea kuhojiwa," alisema.
Alitoa rai kwa wananchi kutokubali kuhudhuria mikutano isiyo na kibali na kuongeza kuwa juzi wabunge wanne wa chama hicho; Lissu (Singida), Mustafa Akonay (Mbulu), Said Arfi (Mpanda Mjini) na wa Viti Maalumu, Joyce Nkya na wafuasi wao 67 walikamatwa na Polisi Soweto kwa kufanya mkutano usio halali na wanafikishwa mahakamani leo.
Chagonja alisema sababu ya polisi kurusha mabomu hayo ni baada ya walinzi wa chama hicho, Red Brigade kumshambulia Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD) ya Arusha na mara polisi walipoona OCD
anashambuliwa walitumia mabomu kutawanya wabunge hao na wafuasi wao ambao walikusanyika bila kibali.
Alisema polisi walishauriana na Mbowe ili azuie wafuasi hao na waondoke uwanjani hapo baada ya wenye uwanja Kituo cha Mikutano ya Kimataifa Arusha (AICC ) kuzuia shughuli za maombolezo viwanjani hapo na kutarajia kuwa Mbowe angewatangazia wafuasi hao watawanyike, lakini hakufanya hivyo na kuendelea na mkutano.
Kuhusu bastola iliyookotwa juzi wakati polisi wakirusha mabomu kutawanya wafuasi hao, Chagonja alisema mhusika alijitokeza jana Polisi na kujitambulisha kuwa mkazi wa Daraja Mbili ambaye hakumtaja jina.
Uchunguzi wa Polisi ulibaini kuwa hajailipia kodi silaha hiyo tangu mwaka 2003 hivyo atatozwa faini na taratibu nyingine zitafuata.
Pia Polisi inaendelea kushikilia magari sita, pikipiki 106 na baiskeli 16 za wafuasi wa chama hicho likiwamo pia gari la Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni (KUB), Mbowe.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Bana alisema ni hatari kwa kiongozi mkubwa wa kisiasa kudai ana ushahidi wa tukio hilo, lakini akagoma kuieleza Polisi na akataka kujua uko wapi uzalendo wa kutanguliza maslahi ya Taifa kwa mtu kama huyo.
Akizungumza na mwandishi jana kwa simu, Dk Bana alisema kila Mtanzania anapaswa kuwa na imani na Jeshi la Polisi kwa kuwa ni chombo cha umma kilichopo kwa mujibu wa Katiba hivyo ni kosa kudai una ushahidi kwa tukio kama lililotokea Arusha lenye sura ya kigaidi, kugoma kuutoa.
Dk Bana alisema hali hii inatia shaka, kwamba ikiwa Chadema wataingia madarakani, wanamaanisha wataunda Polisi yao isiyo na chembe ya Polisi ya sasa na kama sivyo, wanapaswa kuheshimu mamlaka za nchi na sheria zake.
"Jeshi la Polisi lipewe ushirikiano, hasa katika matukio kama haya ya kuudhi, jinai, ugaidi na machafu kwa amani ya nchi yetu, kiongozi kama wa Chadema kudai ana ushahidi lakini hataki kuutoa Polisi, huyu anataka kusaidia kweli nchi yake?," alihoji Dk Bana.
Kutokana na kurushiana maneno kunakoendelea hivi sasa baina ya Chadema na CCM baada ya tukio hilo, Dk Bana alishauri, kwamba huu ni wakati wa vyama hivyo viwili, kukutana na kuzungumza kwa kina kwa usalama wa nchi.
"Natarajia huu ndio wakati wa Chadema na CCM kusahau tofauti zao, nilitarajia yanapotokea mambo kama haya, wangeomba hata kuonana na Rais Jakaya Kikwete Ikulu kama walivyofanya baada ya uchaguzi, badala yake wanarushiana maneno, hii haijengi, wakutane wazungumze," alisisitiza Dk Bana.
Alitoa mwito kwa asasi za kiraia, vyombo vya habari, viongozi wa dini na kijamii, wanaharakati, kujitokeza kwa wingi wakati huu, kukemea haya yanayotokea na kushinikiza wanaosema wana ushahidi wautoe ili kuokoa amani ya nchi inayotaka kuharibiwa na wachache.
"Watanzania hatujajengwa katika mazingira ya kurushiana mabomu, haya ni mambo ya kuchukiza na yanatia hasira, watu wanakufa, leo tunasikia Arusha lakini kesho itahamia Dar es Salaam na kwingineko, kutokuwa na uchungu wa kusaidia nchi ni kukosa weledi.
"Siungi mkono kauli ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye wala ya Mwenyekiti wa Chadema, Mbowe mara baada ya tukio hili, wanarushiana mpira wakati maisha ya Watanzania yanateketea, wakutane kunusuru nchi na watoe ushirikiano kwa vyombo vya Dola," alisema Dk Bana.
Mwenyekiti wa Kigoda cha Taaluma cha Mwalimu Nyerere cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Issa Shivji, aliitaka Serikali kuwa tulivu katika kushughulikia matukio ya kigaidi yanayotokea nchini na kuweka nguvu kubwa kutafuta wahusika badala ya kutumia nguvu hiyo kupambana na vyama vya siasa na wananchi.
Profesa Shivji alisema matukio hayo yana kila dalili ya chokochoko za chini kwa chini zinazofanywa kwa mgongo wa watu wachache kupitia vyama vya siasa, yenye lengo la kuleta machafuko kwa maslahi ya wachache.
Alikuwa akizungumza na gazeti hili juu ya malumbano ya kisiasa baina ya CCM na Chadema yanayoendelea hivi sasa baada ya mlipuko wa pili wa bomu kutokea Arusha.
Alisema: "Binafsi naona hapa wanachanganyana tu, vyama vya siasa vinawachanganya watu na pia vinaichanganya Dola, wanajua ukweli, lakini hawataki kusema, upinzani wanadai wana ushahidi, sasa kwa nini wasifuatwe kwa utaratibu kueleza ushahidi wao?" Alihoji Profesa Shivji.
Aliishauri Serikali kutumia kila namna kuhakikisha inatulia katika kushughulikia matukio haya, la sivyo kuna chokochoko zinazofanywa chini kwa chini, zenye lengo la kuamsha machafuko nchini kwa maslahi ya wachache.
Profesa Shivji anaamini kuna watu nyuma ya matukio haya, wanaojua ukweli halisi wa nini kinaendelea na kuitaka Serikali ambayo anaamini ina Dola yenye nguvu na uwezo wa kumpata mhusika, kujikita kutafuta chanzo badala ya kushughulika na mambo yasiyo na msaada kujua ukweli wa mambo.
Alitumia fursa hiyo, kuomba viongozi wa dini na wasio na dini, kuongeza juhudi kuomba amani ya nchi kwa kuwa, hali ilivyo sasa, watu wanajenga uadui kwa misingi ya vyama vya siasa wakati tatizo ni kubwa zaidi ya vyama hivyo.
Mkazi wa Dar es Salaam, Jacob Malihoja katika maoni yake, alisema "Tusinyoosheana vidole tutakosa nafasi ya kumjua mbaya wetu. Tuwe watulivu, wenye hekima ili Serikali ipate muda wa kulishughulikia. Vinginevyo tutafarakana, tutavuragana na Serikali itajikita kwenye mifarakano badala ya kutafuta mbaya wetu."
Malihoja katika maoni, aliendelea kusema, "tukumbuke Tanzania tumeanza kujizolea maadui wanaotokana na wivu wa amani iliyopo. Wapo maadui wanaotokana na mafanikio ya maendeleo ya Taifa na kukubalika na mataifa makubwa."
Alitolea mfano kwamba ujio wa viongozi wa kimataifa, akiwamo Rais wa China, Xi Jinping na hata matarajio ya ujio wa Rais wa Marekani, Obama, havipaswi kupuuzwa vinaweza kuwa chanzo cha chuki dhidi ya Taifa.
Naye Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Mount Meru, Dk Frida Mokiti, amelaani vitendo vya uvunjifu wa amani na vitisho vya wafuasi wa Chadema, ambavyo vilisababisha kuvunjwa kwa mlango wa gari la wagonjwa na kuvunja lango kuu la kuingilia hospitalini hapo.
Alisema katika tukio hilo la bomu, wafuasi hao wa Chadema, walitishia madaktari na wauguzi wa zamu na kutaka kuchoma moto majengo ya hospitali hiyo, kuwakishinikiza kutibiwa haraka kwa majeruhi wa bomu.
Aliongeza kuwa hospitali haikupata taarifa mapema ya mlipuko huo na hivyo kuchelewa kupeleka gari la wagonjwa kwenye eneo la tukio ili kutoa msaada na kilichotokea ni wafuasi wa chama hicho wakiwa na majeruhi walifika hospitalini na kuanza vitishoĆna kufanya fujo zikiwamo kutishia kuchoma moto magari na majengo ya hospitali hiyo.
Alisema hospitali hiyo haibagui wagonjwa wala haitoi huduma kwa itikadi au imani ya mgonjwa bali kazi yake ni kuhudumia watu wote bila ubaguzi.
Dk Mokiti, aliishukuru Wizara ya Maliasili na Utaliii kwa misaada ya vifaa vyenye thamani ya Sh milioni 120 kwa hospitali zote tatu za Mount Meru, Selian na St Elizabeth.
Alisema pia wamepokea madaktari bingwa kutoka Hospitali ya Moi Kenya, ambao wameongeza nguvu ya kuhudumia majeruhi wa mlipuko huo.
Wakati huo huo, kitendo cha wanasiasa kunyoosheana vidole kuhusu tukio hilo la bomu kimeshutumiwa kuwa kinaweza kuathiri upatikanaji wa wahusika sahihi.
Watu wa kada mbalimbali waliozungumza na gazeti hili, walisema shutuma na mvurugano miongoni mwa wanasiasa, vitasababisha Serikali kujikita katika kutatua mifarakano hiyo badala ya kutafuta mbaya wa Watanzania.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu akizungumza na vyombo vya habari jijini hapa kuhusu sekta ya utalii kuathirika na milipuko ya mabomu Arusha au safari za watalii kusimama,
alisema hali ya usalama Tanzania hususan Arusha ni nzuri na kuomba watalii kuendelea kuja nchini kuona vivutio vya utalii.
Alisema Tanzania kuna amani na ndiyo maana hata Rais wa Marekani, Barack Obama anatarajia kuja nchini na kuongeza kuwa kutokana na amani iliyopo milango ya utalii imezidi kufunguka, kwani hivi sasa watalii kutoka Japan, China, Uturuki na sehemu mbalimbali duniani wanakuja kuangalia vivutio hivyo.
Aliongeza kuwa amani ni muhimu kwa Tanzania hususan Arusha ambalo ndio mlango wa sekta ya utalii na kuwasihi viongozi wa vyama vya kisiasa kuhakikisha wanalinda amani nchini kwani endapo itapotea waathirika wengi wakiwamo wadau wa sekta ya utalii, hoteli, wauzaji mboga na wengine wataathirika kimapato na uchumi kudorora.
Katika hatua nyingine, wananchi wa Arusha na viunga vyake, wanaendelea na shughuli zao za kila siku huku wengine mapema jana asubuhi walifika eneo la Soweto kuangalia vitu walivyokuwa wameangusha juzi.
Mwandishi wa habari hizi, alishuhudia baadhi wakiwapa watoto wa mitaani Sh 500 hadi Sh 1,000 ili kuwasaidia kuangalia kama simu, pochi na vitambulisho vyao kama vipo; wengine walivipata lakini wengine hawakuambulia kitu.
No comments:
Post a Comment