Langa Kileo (msanii wa Hip Hop Tanzania, pichani) amefariki dunia leo hii.
Langa alipelekwa hospitali akiwa hajitambui. Anadaiwa kuwa alikumbwa na
Malaria kali sana, Hali iliyopelekea kukimbizwa Hospitali ya Muhimbili
jana.
Uchunguzi wa chanzo cha kifo chake bado unaendelea.
Msanii Langa aliwahi kutamba na kikundi cha Wakilisha pamoja na witness
na sara ni miongoni mwa wasanii wakongwe wa bongo flava nchini Tanzania.
Mungu amrehemu.
===============
Kwa wasiomjua Langa
Je, unamkumbuka Langa Kileo? Bila shaka hili ni jina maarufu, hasa kwa wadau wa masuala ya burudani wa ndani na nje ya nchi.
Huyu ni mmoja wa matunda ya shindano la muziki la Coca-Cola Pop Stars
mwaka 2004 ambalo washindi wake waliounda kundi la Wakilisha.
Mbali ya Langa, wengine ni Sarah Kaisi `Shaa’ na Witness Mwaijaga
`Witness’. Huo ndio uliokuwa mwanzo wa kung’ara kisanii kwa wakali hao,
ingawa kwa sasa kundi hilo limesambaratika, kila mmoja akitamba kivyake.
Lakini kwa bahati mbaya, mmoja wao, Langa kwa miaka ya hivi karibuni
hakusikika kabisa, jambo lililomlazimu mwandishi wa makala haya
kumtafuta sababu za ukimya wake.
Haikuwa kazi rahisi, lakini hatimaye Langa alipatikana na bila kutafuna
maneno alisema kwamba, alishindwa kufanya kazi baada ya kuwa `teja’
aliyekubuhu.
Yaani alizama katika matumizi ya dawa za kulevya kiasi cha kupoteza kabisa mwelekeo si wa kisanii pekee, bali hata kimaisha.
“Siyo siri, kilichokuwa kimenifikisha katika hali hiyo ni dawa za
kulevya. Kwa miaka mitano nilitumia sana Cocaine, Heroin, bangi na
pombe. Namshukuru Mungu sasa nimerejea katika hali yangu…
“Siamini kama nimenusurika kwa sababu madawa yalinitesa, nikafanya mengi
ya ajabu yaliyoichukiza familia yangu na marafiki ikiwa pamoja na kuwa
mwizi na mkabaji mitaani na nyakati za usiku,” anasema Langa ambaye
kundi lao la Wakilisha lilitamba na nyimbo kama `Unaniacha Hoi’ na
`Kiswanglish’.
Anaeleza kwamba, kwake hayo ndiyo aliyoyaona maisha yanayomfaa, akidai
awali alikuwa amechoshwa kuishi kwa masharti kutoka kwa wazazi wake
waliokuwa wanampa mwongozo wa maisha, lakini bila kujua akadhani
`anachungwa’.
Kwamba, umaarufu na ngekewa ya kuzishika pesa katika umri mdogo kupitia
muziki vilimtia kiburi zaidi, na hivyo kuamua kujitenga kabisa na
familia yake iliyomlea kwa mapenzi mazito.
“Niliamini naweza kujitegemea kupitia kazi yangu ya muziki,
nikajichanganya mtaani,” anasema kijana huyo aliyetoa kibao chake cha
kwanza, Matawi ya Juu mara baada ya kusambaratika kwa kundi la Wakilisha
kutokana na kila mmoja kuamua kujitegemea kimuziki. Na kweli, Matawi ya
Juu ilidhihirisha kuwa Langa ni moto wa kuotea mbali katika fani.
Aliweza kusimama kwa miguu yake na kutikisa.
Mwenyewe anasema: “Jina hilo la Matawi ya Juu lilidhihirisha hivyo pale
video ya kibao hicho ilipotajwa kuwania Tuzo za MTV Base kwa upande wa
hapa Bongo miaka michache iliyopita, kisha kutwaa Tuzo ya Kisima nchini
Kenya. “Moto huo uliwafanya baadhi ya wasanii wakongwe katika gemu ya
Bongo Fleva kunitafuta na kunipa majukumu ya kushiriki katika kazi zao,
ikiwemo Chagua Moja ya Farid Kubanda `Fid Q’.
“Baada ya kuona wakongwe wamekubali vitu vyangu na kuanza
kunishirikisha…nikapata pia safari za nje ya nchi. Huko Nairobi (Kenya)
niliweza kufanya kazi na vichwa vikali vinavyounda Kundi la Necessary
Noise, Naaziz na Wyre (Kevin Wyre)….”
——————————————————————————–
Anasema mafanikio hayo yalimtuma kufyatua albamu yake ya kwanza aliyoipa
jina la Langa, akiamini itampaisha zaidi kimaisha na kimuziki. Hata
hivyo, mambo yalikwenda kinyume. Anasema alipoipeleka sokoni, wauzaji
wakubwa waliigomea, hivyo kumpa wakati mgumu wa kuwaza na hatimaye
kujikuta akiongeza kasi ya matumizi ya dawa za kulevya.
Siyo siri, kugoma kwa albamu yangu sokoni kulichangia kasi ya kutumia
dawa za kulevya…niliona ni njia pekee ya kuondoa mawazo kwa sababu kazi
iligoma, na home (nyumbani) nilishaharibu.
Sikufanya tena kazi kwa umakini na kila kazi niliyoitia haikufanya
vizuri….” Anasema kwamba, baada ya mambo kumwendea mrama, ndipo
alipoanza kuiba vitu nyumbani kwao kwa lengo la kuviuza na inapotokea
amekosa, alidiriki hata kupiga debe katika vituo vya mabasi ili mradi
apate fedha za kununua `unga’.
Haikuishia hapo, kwani anasema alijiingiza katika kundi la wahuni
waliojihusisha na wizi na ujambazi. “Kwa ujumla nilipoteza mwelekeo.
Maisha yangu yakawa ya kutembea na kisu kama kitendea kazi changu katika
wizi,” anasema huku akitikisa kichwa kama ishara ya kujutia matendo
aliyoyafanya kwa msukumo wa madawa ya kulevya. Anakumbuka akiwa mtumwa
wa `unga’, aliingia katika mikasa kadhaa ikiwa pamoja na kupigana na
polisi baada ya kunaswa na dawa hizo haramu.
Katika wizi, chochote alichokikuta mbele yake kilikuwa halali. Anasema
alikwapua vitu magengeni, madukani na hata magari yaliyoegesha vibaya
alinyofoa vioo na mashine zinazosaidia kupandisha na kushusha vioo ndani
ya gari.
“Ni matukio ya aibu. Yanasikitisha…,” anasema Langa anayedokeza kwamba,
akiwa mtumiaji wa `unga’, alikuwa anakutana na wasanii na watu wengine
mashuhuri. Hata hivyo anakataa kuwataja, akidai ni siri yake. `Ufufuo’
wa Langa kutoka katika lindi la mateso ya dawa za kulevya ulipatikana
kuanzia Machi mwaka huu, baada ya familia yake kumpeleka kijana wao kwa
tiba maalumu ya kuachana na matumizi ya `madudu’ hayo. Na kweli, elimu
imemwingia na kujikuta akirejea ufahamu wake wa kawaida.
Ametangaza kuachana na `unga’, pombe, sigara na badala yake amejikita
zaidi katika mazoezi ya kurudisha mwili wake katika hali ya kawaida.
Aidha, amekata shauri la kuirudia fani yake na tayari ana vitu vipya,
Bombokiata na Mteja Aliyepata Nafuu.
Anasisitiza kwamba, kutokana na mateso aliyoyapata, anakusudia katika
siku za baadaye afungue kituo chake cha tiba ya dawa za kulevya ili
aweze kuwaokoa vijana wengine wanaoangamia kutokana na matumizi ya dawa
hizo haramu zinazopigwa vita karibu kote duniani. “Nimenusurika,
namshukuru Mungu.
Nami najipanga kutaka kuwasaidia wengine waachane na mateso ya dawa za
kulevya. Pia nichukue fursa hii kuwaomba msamaha wote niliowakosea kwa
namna moja ama nyingine wakati nikiwa `teja’,” anasema Langa, kijana
mwenye umri wa miaka 25.
Je, historia ya maisha ya Langa ikoje? Anasema Desemba mwaka 1985 jijini
Dar es Salaam akiwa tunda la wanandoa Vanessa Kimei na mumewe Mengisen
Kileo. Alisoma Shule ya Msingi Olympio na Sekondari ya Loyola, zote za
jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo, akiwa kidato cha pili alihamishiwa Kampala, Uganda katika
Shule ya Vienna na baadaye Shule ya Hillside International Academy, huko
huko Uganda. Baadaye alirejea nchini na kujiunga na masomo ya
Stashahada ya Masoko katika Chuo cha Biashara Dar es Salaam (CBE),
Kampasi ya Dodoma.
Huyo ndiye Langa Kileo msanii wa muziki wa kizazi kipya ambaye baada ya
kulewa umaarufu na kujikita katika matumizi ya dawa za kulevya, ameibuka
na kujutia `ujanja pori’, sasa akitaka kujiingiza katika kampeni ya
kuwaokoa vijana wengine waliozama katika `unga’. Anakusudia pia kurudi
darasani kujiendeleza na masomo ya elimu ya juu. Je, atafanikiwa? Kwa
hakika, hili ni jambo la kusubiri na kuona.
No comments:
Post a Comment