Askofu
wa Kanisa Katoliki,Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp
Kardinali Pengo amewataka waumini wa kanisa hilo kutoogopa kifo badala
yake waendelee kwenda makanisani licha ya kuwapo kwa vitisho vya
kushambuliwa.
Pengo
alisema hayo jana katika Kanisa la Mtakatifu Joseph alipokuwa akitoa
sakramenti ya kipaimara na aliwataka wasiwe na hofu lakini waendelee
kumwamini Yesu Kristo kama Mwana wa Mungu.
“Tuendelee
kwenda makanisani,kamwe tusiogope kuuawa,tuwe na imani kwamba Yesu
Kristo ndiye mlinzi wetu na ndiye atuongozaye,”alisema Pengo.
Kardinali
Pengo alisema hata kama vyombo vya dola vitakuwa vimeshindwa
kuwalinda,waumini kamwe wasiache kwenda makanisani kwa ajili ya
kuabudu.
Pengo
aliwataka waumini hao kutolipiza kisasi kutokana na mauaji yaliyotokea
hivi karibuni mkoani Arusha kwani kufanya hivyo ni kwenda kinyume na
mafundisho ya Yesu Kristo.
“Wakristo kulipa kisasi ni kwenda kinyume na mafundisho ya dini ya kikristo na sheria za nchi,” alionya Pengo.
Kauli
hiyo imekuja baada ya watu watatu kuuawa kwa bomu na wengine zaidi ya
60 kujeruhiwa hivi karibuni katika Kanisa Katoliki,Parokia ya Joseph
Mfanyakazi,Olasiti nje kidogo ya jiji la Arusha.
Mauaji
hayo yalitanguliwa na kuuawa kwa Padri Evarist Mushi aliyeuawa
Februari 17 wakati akielekea katika Kanisa la Mtakatifu
Theresia,Zanzibar kuendesha misa.
Pia
Desemba 25 mwaka jana,Padri Ambrose Mkenda alijeruhiwa baada ya
kupigwa risasi watu wasiojulikana wakati akisubiri kufunguliwa geti
nyumbani kwake Zanzibar.
Pengo aliwataka waumini wote kuendelea kusali kwa imani yao na kwamba matatizo yanayojitokeza yasiwakatishe tamaa.
Alisema
hata katika mafundisho, kuna mambo mengi ambayo yalifanywa na baadhi
ya watu ili kumkatisha tamaa Yesu Kristo asitimize malengo yake lakini
baadaye alishinda.
“Vivyo
hivyo waumini yanayojitokeza hivi sasa yasitukatishe tamaa tuendelee
na utaratibu wetu wa siku zote na tutashinda,”alisema Pengo.
No comments:
Post a Comment