Wednesday, May 15, 2013

MIILI YA WATU WAWILI YAOKOTWA KANISANI.

MIILI ya watu wawili akiwemo mtoto wa mchungaji wa kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) lililo kwenye kitongoji cha Rehani, kata ya Tutuo, wilayani Sikonge, Tabora imeopolewa kwenye dimbwi la maji katika mazingira ya kutatanisha.
Mtoto wa mchungaji huyo aliyetambuliwa ni Pascal Yasin (27) na Utukufu Stefano Bugore (16) ambao ni wanafunzi wa kidato cha tatu shule ya sekondari ya Tutuo.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu vifo hivyo, Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Tabora, Edward Bukombe alikiri kupokea taarifa hiyo kutoka kwa watu waliotembelea eneo hilo.
Alisema marehemu hao hawakuwa na jeraha lolote katika miili yao ila mmoja alikuwa akitoka damu puani huku akibainisha kwamba uchunguzi wa awali umeonyesha kwamba marehemu walikuwa wakiogelea kwenye dimbwi hilo.
“Marehemu mmoja alikuwa na nguo ya ndani tu huku mwenzake akiwa na suruali bila shati, hivyo inawezekana walishindwa kuogelea wakazama… kwa sababu hawana alama yoyote ile katika miili yao,” alisema kaimu kamanda huyo.
Kwa mujibu wa Bukombe Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Sikonge amebainisha kuwa marehemu walizama baada ya kushindwa kuogelea hivyo wakanywa maji mengi. Aidha uchunguzi wa tukio hilo unaendelea.
Awali mchungaji wa kanisa hilo wilayani Sikonge, Michael Namba, alisema upo uwezekano watu hao wameuawa kwa vile mchungaji wa kanisa la Tutuo hutumiwa ujumbe wa vitisho.
“Meseji zote za vitisho tunazo na tumetoa taarifa kwa polisi wa hapa Sikonge ili ziwasaidie katika uchunguzi wao, kwani hili lilipangwa… na vitisho hivyo vinaendelea,” alisema mchungaji Michael Namba

No comments:

Post a Comment