Friday, April 26, 2013

RAISI WA KENYA UHURU KENYATTA ATANGAZA MAJINA MAPYA 12 YAMAWAZIRI.


Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta ametangaza majina ya mawaziri wapya 12. Miongoni mwao ni mwanadiplomasia Raychelle Omamo aliyepewa wadhifa wa waziri wa ulinzi. Bado wizara mbili hazijapewa viongozi.

Uteuzi uliotangazwa leo unatimiza idadi ya mawaziri 16 kati ya 18 ambao wataunda baraza la kwanza la mawaziri tangu kuchaguliwa kwa Uhuru Kenyatta kuwa rais.

Wanasiasa wa muda mrefu Charity Ngilu na Najib Balala wamo kwenye orodha iliyotangazwa leo. Ngilu ataiongoza wizara ya ardhi, huku Balala akielekea katika wizara ya madini na migodi. Michael Kamau ndiye waziri mpya wa usafirishaji, wakati mtaalamu wa maswala ya uchumi, Phyllis Chepkoskey Kandie, akipewa wizara ya utalii. David Chirchir amekabidhiwa wizara ya nishati na mafuta.

Maswali juu ya ukabila
Makamu wa rais wa Kenya William Ruto Makamu wa rais wa Kenya William Ruto

Baraza jipya limezusha maswali juu ya namna wengi wa mawaziri walioteuliwa wanavyotoka katika makabila ya Kikuyu na Kalenjin, ya rais Uhuru Kenyatta na makamu wake, William Ruto. Akijibu maswali ya waandishi wa habari juu ya wasiwasi huo, Rais Kenyatta amesema wamejaribu kuweka uwakilishi wa majimbo yote ya nchi kwa kadri ya uwezo wao. ''Kwa bahati mabaya baraza hili sio kubwa kama yale yaliyotangulia,'' alisema Kenyatta.

Jumanne wiki hii, Rais Kenyatta alikuwa ameteua waziri wa fedha, waziri wa mambo ya nchi za nje, waziri wa habari na waziri wa afya. Wizara ambazo bado zinasubiri kujua watakaoziongoza ni ile ya utumishi, usalama wa kijamii na huduma kwa umma, pamoja na wizara ya mambo ya ndani na tawala za majimbo.

Wasiwasi juu ya uteuzi nusu nusu
Amina Mohamed ni miongoni mwa mawaziri wapya, anayeongoza wizara ya mambo ya nje Amina Mohamed ni miongoni mwa mawaziri wapya, anayeongoza wizara ya mambo ya nje

Maswali yamekuwa yakiulizwa kuhusu sababu ya kulitangaza baraza la mawaziri hatua kwa hatua. Mchambuzi wa masuala ya kisiasa kutoka Kenya Bobby Mkangi, ameiambia DW kuwa changamoto kubwa inatokana na utekelezwaji wa makubaliano kati ya rais Uhuru Kenyatta na makamu wake William Ruto, ambayo yanasema vyama vyao vitagawana madaraka nusu kwa nusu.

Kabla ya kupitishwa rasmi, mawaziri wateule watachunguzwa na kamati ya bunge, inayowajumuisha maspika wa bunge na seneti pamoja na wabunge kutoka mabaraza hayo mawili. Hata hivyo, muungano wa kisiasa wa Jubilee wa rais Uhuru Kenyatta na Makamu wake unao wingi wa wabunge katika mabaraza hayo.

No comments:

Post a Comment